Benki ya CRDB imezindua rasmi SME Biashara Club Kanda ya Kaskazini tarehe 9 Octoba 2026 katika ukumbi wa Lush Garden Business Hotel, Jijini Arusha. Tukio hilo limewakutanisha wafanyabiashara mbalimbali wa sekta ya SMEs kwa lengo la kuimarisha mahusiano na benki, kutoa fursa za kujifunza, kupeana uzoefu na kujenga mitandao ya kibiashara itakayochochea ukuaji na ustahimilivu wa biashara zao.

Kupitia jukwaa la CRDB SME Biashara Club, wateja wa SMEs wanapata fursa ya kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa biashara, kupanua mitandao na kupata washirika wapya wa kibiashara, pamoja na kupata elimu ya kifedha na ushauri wa kitaalamu kuhusu bidhaa na huduma za kifedha zinazosaidia ukuaji endelevu wa biashara zao.

Benki ya CRDB inaamini kuwa Jukwaa la CRDB Biashara Club litakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya wafanyabiashara wa Kanda ya Kaskazini na Taifa kwa ujumla, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuendelea kuwasikiliza, kuwawezesha na kusimama na wajasiriamali wa Kitanzania.