
Berla Mundi, ambaye jina lake halisi ni Berlinda Addardey, alianza safari yake ya umaarufu mwaka 2010 aliposhiriki shindano la urembo la Miss Malaika nchini Ghana na kuibuka mshindi wa tatu.
Nafasi hiyo ilikuwa chachu iliyomfungulia milango katika tasnia ya habari, ambapo alianza kufanya kazi kama mtangazaji wa redio na televisheni kwenye kituo cha GHOne TV.
Akiwa hapo, alijizolea sifa nyingi kupitia vipindi kama Rhythmz Live, akionyesha uwezo mkubwa wa kuzungumza na kuvutia watazamaji, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa watangazaji chipukizi waliotabiriwa kufika mbali zaidi.

Hivi sasa, Berla ni gwiji katika tasnia ya habari barani Afrika, akifanya kazi na kampuni kubwa ya Media General (TV3) ambapo anaendesha vipindi maarufu kama The Day Show na New Day.

Zaidi ya utangazaji, amekuwa sura ya matukio makubwa ya kimataifa kama vile Global Citizen Festival na tuzo za VGMA. Kupitia asasi yake ya Berla Mundi Foundation na mradi wa B.You, amejitolea kuwasaidia na kuwanoa wasichana wadogo kifikra, akitumia ushawishi wake kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na kudhihirisha kuwa yeye ni zaidi ya mtangazaji, bali ni kiongozi na mwanaharakati wa maendeleo.