
Taasisi ya Flaviana Matata Foundation (FMF) imekamilisha na kukabidhi mradi wa miundombinu ya maji na usafi katika Shule ya Sekondari Kimara jijini Dar es Salaam. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuelimika kwa wanafunzi wa kike, kwa kuhakikisha wanapata mazingira safi, salama na yenye staha.
Mradi huo umezinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert G. Msando, na umefadhiliwa na wadau na wafadhili wa taasisi hiyo kutoka Marekani. Ujenzi wake unahusisha vyoo 13 vya kisasa maalum kwa wasichana, maeneo ya kunawa mikono yenye maji safi, chumba maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu, chumba cha kujistiri wakati wa hedhi, pamoja na tanki la kuhifadhi maji safi na kichomea taka maalum kwa ajili ya taulo za kike.

Kabla ya uwekezaji huu, Shule ya Sekondari Kimara ilikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa matundu ya vyoo, hali iliyokuwa ikiathiri faragha, afya na usafi wa wanafunzi wa kike. Hali hiyo ilichangia usumbufu mkubwa katika mahudhurio ya masomo, hasa kwa wasichana.
Zaidi ya wasichana 886 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huu kila mwaka. Akizungumza wakati wa makabidhiano, mwanzilishi wa taasisi hiyo, Flaviana Matata, alieleza kuwa ukosefu wa huduma rafiki za WASH ni kikwazo kikubwa kinachowakwamisha wasichana wengi kuhudhuria shule, hasa wakati wa hedhi. Aliwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo adhimu kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.








