Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ametangaza hatua mpya katika juhudi za serikali yake kukabiliana na changamoto ya makazi nchini humo, ambapo nyumba 700 za bei nafuu katika mradi wa Saglemi zinatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa rasmi ifikapo Machi 2027. 

Kwa mujibu wa Rais Mahama, serikali imejipanga kuhakikisha kuwa jumla ya nyumba 1,500 zitakuwa zimekamilika ifikapo Desemba 2027, hatua ambayo itahitimisha awamu ya kwanza ya mradi huo muhimu. 

Mradi wa Saglemi ulianzishwa awali kwa lengo la kujenga jumla ya nyumba 5,000 za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati, lakini kwa miaka mingi umekuwa ukisuasua, ukiwa haujakaamilika na kubaki bila wakazi. 

Serikali ya sasa imesisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, kazi itaendelea kwa kasi ili kuhakikisha nyumba 3,500 zilizobaki zinajengwa na kukabidhiwa kwa wananchi.