
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, ameungana na wazungumzaji pamoja na washirika mbalimbali katika mjadala maalumu wa “Changamoto na Ubunifu katika Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwenye Kilimo na Ufugaji,” uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa COP31.
Mjadala huo uliofunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia na Mwanzilishi wa Taasisi ya YADAM Foundation, Mheshimiwa Ato Demeke Mekonnen, ulilenga kutilia mkazo umuhimu wa kupanua wigo wa suluhisho zinazobuniwa na kuongozwa na jamii zenyewe, kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya kilimo, pamoja na kubuni mifumo mipya ya ufadhili itakayowawezesha wakulima na wafugaji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mbali na kubadilishana maarifa na uzoefu, mjadala huo umeipa CRDB Bank Foundation fursa muhimu ya kuimarisha mahusiano yaliyopo na kujenga ushirikiano mpya wa kimkakati ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Taasisi hiyo imetoa shukrani za dhati kwa waandaaji na washirika wote waliofanikisha ushiriki huo, ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kujenga na kuimarisha ushirikiano utakaosaidia kubadili ahadi na nia njema za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa suluhisho halisi na lenye manufaa ya kudumu kwa jamii.






