
Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, ikishirikiana na Benki ya Absa Tanzania pamoja na kampuni ya Afropavo Limited, imezindua huduma mpya ya kidijitali inayofahamika kama ‘M-Pesa MCHEZO’.
Huduma hii imeundwa maalum kurahisisha uanzishaji na usimamizi wa vikundi vya upatu kote nchini kupitia simu za mkononi, ikiwa ni hatua kubwa ya kuleta mageuzi katika mfumo wa akiba na uwekezaji wa kijamii.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam uliwakutanisha viongozi wa taasisi hizo tatu, ambapo Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa kutoka Vodacom, Tulisindo Mlupilo, alibainisha kuwa mfumo huo utasaidia kuongeza uwazi na uaminifu miongoni mwa wanachama.
Kupitia M-Pesa MCHEZO, washiriki wataweza kutuma michango yao kwa urahisi pamoja na kufuatilia taarifa zote za miamala na rekodi za kifedha kwa njia ya kidijitali bila urasimu au hofu ya kupoteza fedha zao.









