Kampuni ya uchapishaji ya Hearst Magazines imepanga kufunga jarida la kidijitali la Oprah Daily, linalomilikiwa kwa ushirikiano na nguli wa habari Oprah Winfrey, kufikia mwishoni mwa mwaka 2026. Kwa mujibu wa taarifa ya ndani iliyotumwa kwa wafanyakazi mnamo Novemba 18 na kuonwa na jarida la WWD, hatua hii itahitimisha safari ya miaka 26 ya chapa hiyo iliyoanza Aprili 2000 kupitia jarida la O, The Oprah Magazine. 

Jarida hilo la kimaisha, lililoanzishwa na kampuni ya Hearst kwa kushirikiana na Harpo Entertainment ya Winfrey, lilisitisha machapisho yake ya kawaida ya kila mwezi mnamo Desemba 2020 na kuhamia rasmi mtandaoni kama Oprah Daily mnamo Machi 2021 likiwa na huduma ya uanachama wa kulipia pamoja na matoleo maalum ya nakala ngumu.

Katika kipindi chote hicho, jarida hili liliungana na majarida mengine makubwa yaliyoanzishwa na watu weusi kama vile EBONY, JET na ESSENCE, likiwa na mchango mkubwa wa kuwapa nafasi wanawake weusi kama wasomaji, wahariri, na watu waliopamba kurasa za mbele – ikiwemo hatua ya kihistoria ya Septemba 2020 ambapo Winfrey aliachia nafasi yake ya kawaida ya ukurasa wa mbele ili kumuenzi Breonna Taylor.

Tangazo hilo limekuja siku sita baada ya kutolewa kwa orodha ya zawadi ya Oprah’s Favorite Things 2026, ambapo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15, Winfrey aligawa zawadi hizo studio kwa kuwashangaza walezi 120 wakati wa kurekodi The Oprah Podcast inayoruka YouTube. Hata hivyo, bado haijatangazwa ni wapi mwongozo huo wa zawadi wenye umri wa miaka 30 utahamishiwa pindi Oprah Daily itakapofungwa.