
Mfanyabiashara mashuhuri kutoka Nigeria na Mwenyekiti wa kampuni ya Heirs Holdings, Tony Elumelu, ametoa wito kwa bara la Ulaya kuachana na mfumo wa kuchukua malighafi pekee kutoka Afrika na badala yake kuwekeza katika maendeleo ya viwanda barani humo.
Akizungumza katika mkutano wa Castelfalfi Dialogues 2026 uliofanyika Tuscany, nchini Italia tarehe 16 Novemba, Elumelu alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika unapaswa kutoa kipaumbele kwa uchakataji wa ndani, usafishaji wa malighafi na uzalishaji wa bidhaa viwandani ili kuhakikisha thamani kubwa ya kiuchumi inabaki na kunufaisha chumi za Afrika.
Aidha, Elumelu alitaja sekta za nishati, madini muhimu, umeme na rasilimali watu kuwa maeneo makuu ya ushirikiano zaidi. Aliwahimiza wawekezaji wa Ulaya kusaidia mifumo ya uongezaji thamani ili kuimarisha viwanda vya Afrika, akisisitiza kuwa bara hilo linapaswa kuacha kuwa msambazaji wa malighafi pekee na badala yake kuzibadilisha kuwa bidhaa zenye thamani kubwa zaidi.
