Benki ya NMB imezindua rasmi toleo jipya lililoboreshwa la programu tumizi ya NMB Mkononi, ikiahidi urahisi na unafuu wa huduma za kibenki mkononi. 

Kupitia maboresho hayo, wateja sasa wanaweza kukopa hadi shilingi milioni 5 bila dhamana, kufungua akaunti, kununua bando na vifurushi vya simu, kusimamia akaunti za vikundi, pamoja na kununua bima na huduma nyingine nyingi. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuwa NMB Mkononi sasa imeboreshwa kuwa “Super App” yenye uwezo wa kuwafikia wateja wake walioko takribani milioni 10, huku ikifungua fursa mpya kwa vijana wabunifu kuunganisha suluhisho zao za kidijitali kwenye mfumo huo. 

Zaipuna aliongeza kuwa benki hiyo inalenga kuwakaribisha wabunifu kutoka maeneo mbalimbali kushiriki kuendeleza huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wa kisasa, hatua itakayoongeza ubunifu na kuboresha uzoefu wa mtumiaji.