Google kwa ushirikiano na mwigizaji na mjasiriamali Mwingereza Idris Elba wamezindua mpango mpya wa dola milioni moja unaolenga kuwapa waundaji maudhui 100,000 barani Africa ufikiaji wa bure wa zana za akili bandia, zikiwemo Gemini na bidhaa nyingine za kidijitali.

Mpango huo unalenga hasa waundaji katika nchi tano, Nigeria, Africa Kusini, Ghana, Kenya na Sierra Leone, kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha maudhui yenye ubora wa hali ya juu kwa haraka zaidi na kwa gharama nafuu. Ni hatua inayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika namna maudhui yanavyoundwa na kusambazwa barani Africa.

Ushiriki wa Elba unaendana na dhamira yake ya muda mrefu ya kukuza mfumo wa burudani Africa, ikiwemo mipango yake ya kujenga miundombinu mipya ya ubunifu nchini Ghana na Zanzibar. 

Hatua hii inakuja wakati sekta ya vyombo vya habari na burudani Africa ikiendelea kukua kwa kasi, na makadirio yanaonyesha inaweza kufikia thamani ya dola bilioni 118 ifikapo mwaka 2031, ikichochewa na upanuzi wa intaneti na ongezeko kubwa la mahitaji ya maudhui ya kiasili.