Benki ya NMB imesaini makubaliano ya kimkakati ya ufadhili na Benki ya Maendeleo ya China (CDB) yenye lengo la kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) nchini Tanzania. 

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilimhusisha Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, Huang Zhiqiang. 

Hatua hii inalenga kupanua fursa za upatikanaji wa mitaji kwa sekta hiyo, ikiwawezesha wajasiriamali kupanua biashara zao, kuongeza tija, kutengeneza fursa mpya za ajira, na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Ushirikiano huu pia unatajwa kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na China, ukifungua milango mpya ya fursa za kibiashara na kuimarisha sekta ya SMEs kama mhimili mkuu wa mageuzi ya kiuchumi. 

NMB imesisitiza kuwa dhamira hii inaenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiamini kuwa uwezeshaji wa biashara ndogo na za kati ndio msingi wa kujenga uchumi jumuishi na taifa lenye ustawi zaidi.