
Katika mahojiano ya hivi karibuni na jarida la GQ, mwanamuziki na mfanyabiashara mashuhuri Jay-Z ametoa mtazamo kuhusu jinsi ya kukabiliana na chagamoto za maisha, akisisitiza kuwa kila jambo linalotokea halitokei kumuumiza mwanadamu bali kumjenga.
Jay-Z anafafanua kuwa siri ya mafanikio na amani ya moyo iko katika kuelewa tofauti kati ya kuona maisha yanakushambulia na kuona maisha yanakupatia fursa ya kukua. Jayz akizungumza na GQ alisema, “Kila kitu katika maisha yako hakitokei kwako, kinatokea kwa ajili yako,” akihimiza watu kutoipita kauli hiyo haraka bila kuitafakari, kwani kubadili namna unavyohusiana na matukio ndiyo msingi wa kubadili hatima yako.

Aidha, Jay-Z alieleza kuwa dhana za “kizuri” au “kibaya” ni tafsiri tu za kibinadamu, lakini kiuhalisia maisha ni mfululizo wa matukio yanayotokea bila ubaguzi. Kwa mujibu wa Jay-Z, badala ya kukwama katika malalamiko pale mambo yanapokwenda kuharibika, ni muhimu kukubali ukweli kuwa “mambo hutokea” na kuitumia kila hali kama darasa la kukuimarisha.
