
Tatizo kubwa linalowakumba wafanyabiashara wengi leo sio ubora wa bidhaa. Unaweza kuwa na bidhaa bora kuliko zote sokoni, huduma ya kipekee, na bei nzuri, lakini kama watu sahihi hawajui kama upo, biashara yako itabaki kupambana.
Wengi hudhani changamoto yao ni mtaji au ushindani, kumbe changamoto halisi ni kutokuonekana. Huwezi kutarajia mtu atoke nyumbani kwake aje kununua kwako kama hajawahi hata kusikia jina la biashara yako. Kutokuonekana ndio kunaua biashara nyingi kimya kimya.
Ukweli ni kwamba kama watu sahihi hawajui upo, hawawezi kununua kwako, hawawezi kukupendekeza kwa wengine, na zaidi ya yote hawawezi kukuamini. Kujenga uaminifu katika biashara huanza pale mtu anapokuona mara kwa mara.
Mteja wa leo hanunui tu bidhaa, ananunua uaminifu. Ndio maana kampuni kubwa haziachi kujitangaza hata zikiwa maarufu – zinajua kuwa nje ya macho, nje ya akili. Kila unapojificha, unampa mshindani wako nafasi ya kuchukua wateja wako.
Na hapa ndipo wengi hukosea: kuonekana sio tu kuchapisha post kwenye Instagram au kupost status WhatsApp kila siku. Kuonekana ni kujipanga kimkakati. Ni kuhakikisha biashara yako ipo pale ambapo fursa zinaweza kuikuta.
Je, ukiandikwa jina la huduma yako Google, unaonekana? Je, ukitafutwa kwenye mitandao ya kijamii, unaonekana wa kuaminika? Je, wateja wako wa zamani wanakumbuka kukuongelea?
Mwonekano wa Biashara ni mchanganyiko wa mtandao sahihi, ujumbe sahihi, na mbele ya watu sahihi. Acha kufanya biashara gizani. Toka, jionyeshe, Jiweke mahali sahihi.
