
Mwigizaji maarufu wa Hollywood mwenye tuzo ya Oscar, Viola Davis na mumewe, Julius Tennon, wameonyesha mfano wa kuigwa wa kurudisha fadhila kwa jamii kwa kuwekeza kiasi kikubwa cha dola milioni 1.2 kupitia taasisi yao ya kutoa misaada isiyo ya kifaida ya Davis-Tennon Foundation.
Uwekezaji huo unalenga ujenzi wa kituo kipya cha kisasa cha jamii katika mji alipozaliwa na kukulia huko Central Falls, Rhode Island, ambacho kimepewa jina la heshima la mama yake marehemu, Mary Alice Davis, kama ishara ya kumuenzi kwa malezi na mapambano yake.
Kituo hicho cha Mary Alice Davis kinatarajiwa kuwa faraja na matumaini mapya kwa wakazi kwa kutoa huduma muhimu kama vile msaada wa kijamii kwa familia, fursa za elimu kwa watoto na vijana, programu za kuwawezesha wanajamii na ugawaji wa chakula, huku kikifanya kazi kama mtandao jumuishi utakaowaunganisha wananchi na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza urasimu unaowakabili familia nyingi.
