Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania limemteua mwanamuziki maarufu, mtunzi wa nyimbo na mtetezi wa vijana, Abigail Chams, kuwa Balozi wake mpya wa Kitaifa.

Uteuzi huo umetangazwa jana ofisini kwa UNICEF Dar es Salaam, wakati wa shughuli za mpango wa Girls Takeover kuelekea Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. Katika shughuli hiyo, Kuruthum Massiro kutoka Mkoa wa Mwanza alipata nafasi ya kipekee ya kuhudumu kama Mwakilishi wa UNICEF kwa siku moja na kukutana na Abigail ana kwa ana.

Uteuzi huu unakuja baada ya miaka sita ya Abigail kuhudumu kama Youth Advocate wa UNICEF, akitumia jukwaa lake kupaza sauti ya haki za wasichana, afya ya akili na mabadiliko chanya kwa vijana.

Katika wadhifa wake mpya, Abigail anatarajiwa kutumia muziki na ushawishi wake kuhamasisha ulinzi wa mtoto, kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, kuzuia ndoa za utotoni na kuwawezesha vijana. Pia atakuwa mstari wa mbele kwenye kampeni mpya ya #HaukoSolo inayohimiza vijana kuzungumza na kutafuta msaada kupitia namba ya msaada ya watoto 116.

Hongera sana Abigail! 👏🏽