Adekunle Gold, kupitia taasisi yake ya Adekunle Gold Foundation, tarehe 20 Juni, 2026 aliongoza huduma ya kila robo mwaka ya matibabu ya ugonjwa wa sickle cell katika Kituo cha Matibabu cha Akerele, Surelere, Lagos, ambapo zaidi ya watu 500 wanaoishi na hali hiyo walipata msaada wa kimatibabu 

Huduma hiyo iliyofanyika kwa ushirikiano na SAMI (Sickle Cell Advocacy & Management Initiative) iliashiria maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya sickle cell, na mamia ya wanufaika walipatiwa huduma mbalimbali zikiwemo ushauri wa wataalamu, vipimo vya maabara, udhibiti wa maumivu na dharura, pamoja na ugawaji wa dawa za kuwasaidia kwa muda wa hadi miezi mitatu. 

Nyota wa muziki duniani Adekunle Gold alihudhuria tukio hilo ambapo alizungumza na wanufaika na kutoa ujumbe wa pongezi, akiwatia moyo watoto na wazazi wao: 

“Kama shujaa, niliambiwa mara nyingi siwezi kufanya mambo mengi kwa sababu ya hali yangu, lakini sikuwasikiliza. Leo, nataka kuwakumbusha kuwa mnaweza kuwa chochote mnachotaka kuwa na ndoto zenu ni halali.” 

Aliongeza kuwa lengo la Adekunle Gold Foundation ni kuondoa unyanyapaa dhidi ya ugonjwa wa sickle cell, kuleta uelewa zaidi, na kutoa msaada muhimu kuwezesha kila shujaa kuishi maisha yenye utimilifu.