
Benki ya Equity Tanzania imezindua rasmi tawi lake la 20 jijini Kigoma, ikiwa ni hatua kubwa katika mkakati wake wa kusogeza huduma bora za kifedha karibu na wananchi.
Uzinduzi huo unalenga kuongeza nguvu katika kuchochea fursa za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, hususan kwenye sekta muhimu za biashara, kilimo, uvuvi na uwekezaji, huku uongozi wa benki hiyo ukipongeza juhudi na mshikamano wa timu ya tawi hilo jipya katika kuhudumia wateja.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity, Dkt. Florens Martin Turuka, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Prosper Gunz Nambaya.
Kupitia upanuzi huu wa kufikisha matawi 20 nchini, benki hiyo imeweka wazi dhamira yake ya kuendelea kuunganisha jamii na fursa, kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania.




