Kampuni ya Google imetangaza mpango mpya wa kuweka mfumo utakaowaelekeza watumiaji moja kwa moja kwenye namba za simu za dharura za afya ya akili pindi mazungumzo yao yanapoashiria hatari ya kujidhuru au kujiua. 

Mfumo huu utampa mtumiaji fursa ya kuchagua njia rahisi ya kupata msaada, iwe ni kwa njia ya soga (chat), kupiga simu, kutuma ujumbe wa maandishi, au kutembelea tovuti rasmi ya mashirika yanayotoa huduma za ushauri wa dharura.

Sambamba na maboresho hayo ya kiteknolojia, Google imeahidi kutoa kiasi cha dola milioni 30 za Kimarekani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kusaidia vituo vya dharura kote ulimwenguni. 

Fedha hizo zinalenga kuongeza uwezo wa vituo hivyo katika kutoa huduma za haraka na salama kwa watu wenye uhitaji, huku ikihakikisha kuwa msaada wa kisaikolojia unapatikana kwa urahisi zaidi katika jamii za kimataifa.