Mfanyabiashara, mwanamitindo na msanii maarufu wa Tanzania Hamisa Mobetto amepewa heshima kubwa baada ya kuteuliwa kuwa Bingwa wa Kimataifa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Katika nafasi hiyo mpya, Hamisa atakuwa na jukumu la kuhamasisha matumizi salama, yenye uwajibikaji na yenye usawa ya teknolojia na mitandao ya kijamii, kwa msisitizo maalum kwa wanawake na wasichana ambao ndio wahanga wakubwa wa unyanyasaji wa mtandaoni.

Akizinduliwa rasmi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Hamisa aligusia kwa uwazi giza alilowahi kuliona kwenye mitandao, akisema amewahi kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia wa kidijitali, uvumi wa uongo na mashambulizi ya kashfa yaliyomgusa kama mwanamke.

“Nimeupitia upande wa giza wa mitandao ya kijamii. Najua jinsi maneno, uzushi na mashambulizi ya mtandaoni yanavyoweza kumuumiza mwanamke,” alisema.

Aliongeza kuwa uzoefu wake huo ndio chachu ya dhamira yake ya kutetea wengine, akisisitiza kuwa anataka kuwa sauti ya binti yule ambaye bado hajapata ujasiri wa kutumia sauti yake kujilinda na kujieleza katika nafasi za kidijitali.

Hongera sana Hamisa! 👏🏽