
Nyota wa soka wa kimataifa wa Senegal, Sadio Mané, amewekeza kiasi kikubwa cha dola milioni 20.4 za Marekani katika mradi wa kilimo cha viwanda wa SM10 Agro unaotekelezwa kijijini kwake Bambali, katika mkoa wa Casamance, kusini mwa Senegal.
Mradi huo wa kihistoria unaolenga uzalishaji na uchakataji wa maembe unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa wakazi wa Bambali na maeneo jirani. Kwa ukubwa wa hekta 500, shamba hilo la kisasa linakadiria kuchakata hadi tani 8,500 za maembe kila mwaka, huku likiwa na viwanda vya kisasa vya kuzalisha juisi, djamu na bidhaa nyingine za maembe zenye thamani ya juu, badala ya kuuza mazao ghafi.

Kwa mujibu wa mpango huo, SM10 Agro itazalisha zaidi ya ajira 1,000 za moja kwa moja na mamia ya ajira nyingine zisizo za moja kwa moja katika mnyororo mzima wa thamani, kuanzia kilimo, uvunaji, usafirishaji hadi uuzaji. Hii itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo wa eneo hilo.

Kwa Mané, ambaye alikulia Bambali kabla ya kung’ara katika soka la Ulaya, mradi huu ni zaidi ya uwekezaji wa kibiashara. Ni kurudisha fadhila kwa jamii iliyomlea na kuunganisha mafanikio yake uwanjani na mizizi yake. Hatua hii inaonesha dhamira yake ya muda mrefu ya kuleta maendeleo endelevu, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kujenga uchumi imara nyumbani kwake Casamance.
