
Kampuni ya kutengeneza bidhaa za utunzaji wa ngozi ya DECIEM imetangaza ushirikiano na mashirika mbalimbali ya damu – yakiwemo Canadian Blood Services, New York Blood Center, NHS Blood and Transplant, pamoja na Bloddonorerne Svendborg ya Denmark – ili kuhamasisha uchangiaji wa damu na upatikanaji wa elimu juu ya suala hilo.
Katika taarifa yake, kampuni hiyo ilisema falsafa yao imejikita katika kuhakikisha huduma zinakuwa rahisi kufikiwa na wote, huku wakisisitiza kuwa ingawa baadhi ya makundi yamekuwa yakitengwa kuchangia damu kwa misingi ya utambulisho wao jambo ambalo hawakubaliani nalo, bado wanaamini uchangiaji damu ni muhimu sana.

Kampeni hiyo itahusisha matukio ya kuchangia damu yatakayofanyika Novemba 27 katika maeneo mbalimbali, ikiwemo 575 Fifth Avenue jijini New York kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 11 jioni, na 18 Distillery Lane jijini Toronto kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 9 alasiri.
Hatua hii inafuatia kampeni ya awali ya chapa yake ya The Ordinary iliyotumia maduka bandia ya vyakula kupinga gharama kubwa zisizo na msingi katika sekta ya urembo kwa kuweka bei za juu kupita kiasi kwenye mahitaji ya kawaida ya kila siku.
Kwa mara nyingine tena, msimamo wa kila mwaka wa kampuni hiyo wa kupinga manunuzi ya ghafla na yasiyo ya lazima unakuja na mwaliko wa kipekee na wa vitendo kwa jamii: kujitolea kitu chenye thamani ambacho hakiwezi kuwekwa kwenye kikapu cha manunuzi.
