Yvonne Okwara, mtangazaji nguli kutoka nchini Kenya, amejiunga na shirika la kimataifa la Shuga Global kama Mkuu wa Uwekezaji na Ushirikiano. Uteuzi huu unafungua ukurasa mpya katika taaluma yake mara tu baada ya kutangaza kustaafu kwenye ulingo wa uandishi wa habari uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Shuga Global Jumatano, Oktoba 28, Okwara ametajwa kama mtaalamu mahiri wa mawasiliano ambaye uzoefu wake unavuka mipaka ya chumba cha habari. Shirika hilo limemtaja kama kiongozi mwenye uwezo mkubwa katika mawasiliano ya kimkakati ya mashirika, uchangishaji wa fedha na usimamizi wa uhusiano na serikali.

Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa ya kitaaluma kwa mwanahabari huyo, kutoka kwenye ulimwengu wa habari na mijadala ya kisiasa kuelekea kwenye nyanja ya uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano wa kimaendeleo. Wengi wanaona ujio wake Shuga Global kama nyongeza ya thamani kubwa, kutokana na ushawishi, weledi na uaminifu alioujenga kwa miaka mingi akiwa mbele ya kamera.

Hongera sana Yvonne! 👏🏽