
Biashara ndogo nyingi hazifi kwa kukosa wateja, zinakufa kwa kushindwa kutunza pesa ya kila siku. Kosa kubwa tunalofanya wote ni kuchanganya pesa ya biashara na pesa ya matumizi ya nyumbani.
Ukichanganya hivi hutaweza kujua kama unapata faida au unafanya kazi bure. Lazima utenganishe kuanzia siku ya kwanza, hata kama biashara yako ni ndogo.
1. Andika kila shilingi inayoingia na inayotoka
Usitegemee kumbukumbu ya kichwa. Kila mteja akilipa andika papo hapo kwenye daftari au simu. Andika hata matumizi madogo kama nauli ya 2,000 au vocha. Mwisho wa siku kaa dakika 10 jumlisha mauzo yote na gharama zote ujue umebakisha ngapi.
2. Tenganisha pesa ya biashara na pesa ya nyumbani
Hii ndio sababu biashara nyingi hazikui. Usiweke pesa yote mfukoni mmoja. Tumia Lipa Namba tofauti kwa biashara na usitoe pesa ya biashara kwa matumizi ya chakula au starehe. Pesa ya biashara ibaki kwa ajili ya biashara tu.
3. Gawa faida kila siku unapofunga
Ukifunga biashara gawa pesa mara moja. Weka kando mtaji wa kesho usiuguse, weka kando pesa ya kodi na usafiri, na kile kinachobaki hata kama ni 5,000 peleka kwenye akiba yako pembeni. Ukifanya hivi kila siku hutakosa mtaji wa kuongeza mzigo na hutalazimika kukopa.
