Kutunza pesa ni changamoto kwa watu wengi, si kwa sababu ya kipato kidogo, bali kwa sababu ya kukosa mpango. Mara nyingi pesa inaingia leo na kesho inakuwa imetumika bila kujua imeenda wapi. Ukweli ni kwamba kutunza pesa si suala la kuwa na kipato kikubwa, ni suala la tabia na nidhamu ya kila siku.

Hatua ndogo unazochukua leo ndizo zinazojenga utulivu wa kesho. Akiba inakupa amani ya akili, inakusaidia kukabiliana na dharura bila hofu, na inakufanya uwe na uwezo wa kutimiza malengo yako makubwa bila kukopa. Huhitaji kuanza na kiasi kikubwa, unahitaji tu kuanza na mpango. Hizi hapa ni njia tatu za msingi zitakazokusaidia kuanza safari yako ya kutunza pesa kwa uhakika.

1. Fuatilia Kila Inapoenda

 Huwezi kutunza usichokijua. Anza kuandika kila kinachoingia na kila kinachotoka kila wiki. Tenganisha matumizi yako – gharama za lazima, msaada kwa familia, na starehe. Utaona wazi wapi pesa inapotea na utaweza kufanya maamuzi bora.

2. Tumia Pesa Kwa Busara

Kabla ya kutumia au kutuma pesa, usikurupuke. Linganisha gharama, angalia makato yaliyofichika na usalama wa njia unayotumia. Epuka manunuzi ya ghafla na njia zisizo rasmi. Kila shilingi unayookoa kwenye gharama ni shilingi inayorudi kwenye akiba yako.

3. Weka Malengo Yaliyo Wazi

Akiba bila lengo ni rahisi kutumika. Lengo linahitaji kiasi na tarehe. Weka lengo dogo la muda mfupi na lengo kubwa la muda mrefu. Andika malengo yako na yagawanye katika hatua ndogo, hivyo kutunza pesa kunageuka kuwa tabia ya kila siku.