Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama, anatarajiwa kuandaa podcast mpya inayojikita kwenye vitabu sita ambavyo ameeleza vimechangia kwa kiasi kikubwa kuunda mtazamo wake wa dunia. Podcast hiyo inaitwa “A Great Book with Barack Obama” na inatarajiwa kuzinduliwa kwa kipekee kupitia mtandao wa Audible mnamo Septemba 24.

Mradi huu ni ushirikiano kati ya Audible na kampuni ya utangazaji ya Higher Ground, iliyoanzishwa na Obama na mkewe, Michelle Obama. Katika kila moja ya vipindi sita, Obama atajadili kitabu kimoja kati ya hivyo sita akiwa na mgeni maalum, akichambua ujumbe na athari zake.

Vitabu alivyovichagua ni pamoja na The Fire Next Time cha James Baldwin, Song of Solomon cha Toni Morrison, All the Pretty Horses cha Cormac McCarthy, Gilead cha Marilynne Robinson, All the King’s Men cha Robert Penn Warren, na Tinker, Tailor, Soldier, Spy cha mwandishi wa riwaya za ujasusi kutoka Uingereza, John le Carré.

Akitangaza podcast hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Obama alisema, “Wakati ambapo watu wachache wanaweza kukaa na kusoma kitabu, ni muhimu kukumbuka furaha na nguvu inayokuja na usomaji. Na baadhi ya vitabu havisimulii tu hadithi – hubadilisha jinsi tunavyouona ulimwengu.” Aliongeza kuwa vitabu vikubwa vimekuwa vikimsaidia kuelewa yeye ni nani na anaamini nini, na kila kimoja kina kitu cha kutufundisha kuhusu uzoefu wa kibinadamu.